TAARIFA YA JESHI LA POLISI KUHUSU BASI LILILOPIGWA BOMU MKOANI KIGOMA NA WATU WANAOSADIKIWA KUWA NI MAJAMBAZI KUTOKEA BURUNDI
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu
WATU watatu wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kulirushia bomu basi dogo la abiria.
Tukio hilo la kutisha lilitokea jana katika Kijiji cha Kilelema, Kata ya Kilelema, Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, dereva wa basi hilo namba T 570 CBE, Benedict Emmanuel, alisema basi lake lilipigwa bomu jana saa 12:15 alfajiri alipokuwa akitoka Kilelema kwenda mjini Kasulu.
“Kabla ya kupigwa bomu hilo, tulifika katika pori la Kasesema ambalo lina historia ya matukio ya uhalifu kwa kipindi kirefu.
“Tulipofika katika pori hilo lililoko Kilelema, niliona kwa mbali watu wawili wakiwa wamesimama barabarani. Kwa hiyo nilichokifanya, niliwawashia taa kali nikidhani ni watu wa kawaida.
“Mmoja kati yao, alikuwa mbele kidogo kwenye kona, nikaona kama ana silaha lakini sikumjali sana, kwa hiyo nilijipa moyo ili niwapite kwa kasi.
“Wakati nikiendelea kuwafikiria watu hao, ghafla niliwafikia na hapo nikasikia mlio mzito kama wa bomu limepigwa nyuma ya basi upande wa kushoto.
“Yaani nilichanganyikiwa, nikataka kusimama, lakini abiria wangu wakasema ongeza spidi hao ni majambazi wametupiga bomu,” alisema Benedict na kuongeza:
“Nilikanyaga mafuta kwa nguvu nikafanikiwa kuwaacha mbali hadi nilipofika katika Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Migongo nikasimama.
“Nilipofika hapo kambini tukakuta abiria wawili wamefariki dunia na mmoja hali yake ilikuwa mbaya sana.
“Kwa hiyo, tulitoa taarifa kwa mkuu wa kambi hiyo ya jeshi naye akawapigia simu polisi ambao walikuja na taratibu za kuwapeleka majeruhi katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu zikafanyika,” alisema.
Kwa mujibu wa Benedict, eneo walipopigiwa bomu ni la hatari kwa kuwa wahalifu kutoka Burundi huteka magari ya abiria mara kwa mara.
“Eneo hilo ni la hatari kwa sababu Warundi wanafanya uhalifu mara kwa mara na wanapomaliza kufanya hivyo, wanarudi kwao kwa sababu hapo ni jirani sana na Burundi,” alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kilelema, Benedicto Mahuta, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Buhigwe, SamwelI Utonga, alithibitisha kutokea tukio hilo.
Alisema watu hao wanaosadikiwa ni majambazi, mara nyingi hutokea Burundi.
“Ni kweli kuna basi ya Hiace imepigwa bomu na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi kutoka Burundi.
“Eneo lilikotokea tukio hilo ni hatari kwa sababu matukio ya uhalifu yanatokea mara kwa mara na abiria huporwa mali kwa kutumia silaha.
“Lakini bado tunaendelea na upelelezi kuangalia namna ya kuwapata watu hao,” alisema Utonga.
Kwa muda mrefu Mkoa wa Kigoma umekuwa ni kati ya mikoa inayoripotiwa kuwa na matukio ya uhalifu wa kutumia silaha unaodaiwa kuhusisha raia wa nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Kutokana na hali hiyo, viongozi wa Serikali ya Tanzania na nchi hizo wamekuwa wakikutana mara kwa mara kujadili jinsi ya kukabiliana na wahalifu hao.
Mtanzania