Hatimaye mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam yameanza
safari zake rasmi leo, Mei 10 kwa kuwasafirisha wananchi bure siku
mbili mfululizo ambapo mpaka Mei 12 ndiyo wataanza kulipia huduma hiyo
ya usafiri.
Mabasi hayo yameanza safari zake kwa barabara mbili kubwa, kuanzia
Morocco mpaka Kivukoni na kutoka Mbezi Mwisho mpaka Kivukoni. Wananchi
wengi wameonekana kufurahishwa na mabasi hayo ambayo yameonekana
kurahisisha usafiri kwa kutoka muda mwingi vituoni lakini wengi
wameonekana bado wakiendelea kulalamikia nauli kuwa kubwa pindi
watakapoanza kulipia huduma hiyo itakuwa ni shida kwao.
Aidha mabasi hayo yameonekana kujaza muda wote wa safari huku abiria
wengi wameonekana wakizunguka na mabasi hayo pasipo kushuka na kuwaacha
wale wanaosafiri kweli kupata shida kwenye vituo hivyo.
Hata hivyo mabasi hayo yatakuwa na mifumo miwili ya ulipiaji wa
nauli, mfumo wa kwanza ukiwa ni kulipia kwa tiketi kununua kwenye vituo
vya kupandia mabasi hayo na mwingine ukiwa ni wa kulipia kwa kutumia
kadi.
“Mfumo wa kadi ndiyo mfumo sahihi wa mabasi haya ila huu wa tiketi
tumeuweka kwa dharura ili kuwasaidia wananchi lakini baada ya muda
utaondolewa. Kuanzia kesho kadi zitaanza kuuzwa kwa shilingi 4500,
lakini ndani yake kutakuwa na bonasi ya shilingi elfu mbili,” alisema
mmoja wa viongozi wa kwenye vituo hivyo.
Aliongeza kuwa, “hiyo kadi ukinunua unatakiwa uanze kuiwekea hela na
ukifika kwenye kituo unaingiza kadi kwenye mashine itakuruhusu uingie.”
Nauli za mabasi hayo itakuwa kama ifuatavyo; Mbezi Mwisho mpaka
Morocco itakuwa ni shilingi 800, Mbezi Mwisho mpaka Kariakoo ni shilingi
800, Morocco mpaka Kivukoni ni shilingi 650, Kariakoo mpaka Morocco ni
shilingi 650, Mbezi Mwisho mpaka Kivukoni ni shilingi 800 na nauli ya
wanafunzi ni shilingi 200.
Tazama picha zaidi hapo chini.
No comments:
Post a Comment