Wiki hii mioyo yetu inaweza kuwa imeanza kupoteza matumaini kwa dada yetu, Rehema Chalamila, wamjua zaidi kama Ray C au kama ukitaka kumpa jina lenye sifa zake, basi yafaa umuite ‘Kiuno Bila Mfupa.’
Ni baada ya kusambaa video inayomuonesha akiwa katika hali inayosikitisha akibebwa kwenye gari la polisi, si kwa kutenda kosa, bali kwa kumuokoa kutoka kwenye hatari ya kujidhuru yeye mwenyewe.
Inadaiwa kuwa muimbaji huyo alionekana akipiga kelele, kujitupa kwenye matope na kutafuta kisu ajichome. Hali aliyofikia Ray C inatisha na kiukweli vita yake dhidi ya uraibu wa madawa ya kulevya imekuwa ndefu, ngumu, inayokatisha tamaa na ni kama sasa ameamua kuweka silaha chini, ameshindwa.
Kwa kauli yake mwenyewe, Rehema alidai kuwa arosto wanayopata mateja si ya mzaha na ndio sababu kubwa inayowafanya washindwe kuacha. Mwili huuma kama unapondwa na kitu kizito, mambo hayendi bila kupata starter ya unga na kwao kuishi na arosto ni sawa na kuianza jehanamu kabla ya wakati. Hupata mateso makubwa na kwakuwa uraibu huo hauhusishi mwili tu, bali hisia na kisaikolojia, wengi hushindwa kuhimili nguvu yake.
Miaka mitatu iliyopita, Ray C aliacha kabisa madawa ya kulevya na kuwa mtetezi mkubwa na muhimu wa waathirika wa unga. Alianzisha taasisi yake na akawa anawatembelea waathirika wa madawa hayo akiwemo yule dada aliyekuwa model kwenye video ya Ice Cream ya Noorah. Ray C akawa ‘bad girl gone good’ na kuwa mvuvi mzuri wa mateja aliowahimiza kwenda kuchukua dawa ya Methadone aliyokuwa akitumia pia.
Baada ya miaka miwili, tetesi za kuwa amerejea tena kwenye matumizi ya madawa hayo, zikarudi. Alizikana vikali na kutishia kuishtaki kampuni ya Global Publishers iliyoandika habari hiyo. Ni hadi wiki hii iliposambaa video hiyo kila mtu akaamini tetesi hizi kumbe ni za kweli.
Wakati wengi wakitoka machozi ya huruma kwa Ray C na wasijue watamsaidiaje awamu hii, kuna matumaini mapya kwa Chidi Benz, kipaji kingine kilichopotezwa na uraibu.
Chidi Benz amewahi kujaribu njia nyingi na za aina tofauti tofauti za kutaka kujiondoa kwenye matumizi ya madawa hayo. Amewahi kwenda Kenya ambako swahiba wake Nonini alitumia gharama kubwa kufanya process ya kitaalaam kumsaidia lakini ilishindikana. Inasemekana pia kuwa Diamond amewahi kumsaidia katika hilo lakini walichemka.
Chidi amepitia mengi ya kutisha zaidi katika utumiaji wa madawa ya kulevya huku akiwa msanii wa kwanza kuwahi kushtakiwa na kesi ya kukutwa nayo. Kesi yake ya kukamatwa na madawa ya kulevya kwenye uwanja wa ndege wa JNIA akielekea Mbeya iligeuka kuwa jinamizi ambalo kama angecheza lingempeleka jela.
Mungu alimsaidia kwa kupewa hukumu iliyokuwa na option ya faini na akawa mtu huru. Baada ya hapo Chidi akawa kimya tena licha ya kuwahi kutoa wimbo aliowashirikisha Diamond na AY. Alikuja kuwashtua mashabiki wa muziki miezi kama miwili iliyopita baada ya kuonekana kwenye interview na kipindi cha D’Weekend Chatshow cha Clouds TV ambapo afya yake ilikuwa ya kutisha.
Chidi hakuwa tena yule rapper mwenye mwili wa miraba minne. King Kong alikuwa amedhoofika utadhani mgonjwa wa Kifua Kikuu. Muonekano huo uliwatisha watu wengi na hivyo kumfanya Babutale aingilie kati na kumpeleka kwenye kituo cha kusaidia waathirika wa madawa ya kulevya cha Life and Hope Rehabilitation akishirikiana na Kalapina.
Fast forward.. Chidi ametoka na wiki hii ameonekana akiwa na muonekano tofauti unaotia moyo. Kupitia akaunti yake mpya ya Instagram, Chidi ameanza kurudisha matumaini mapya na kiukweli mashabiki wamefurahi. “Kesheni mkiniombea. Trust me, Your kingkong is coming back soon,” ameandika kwenye picha moja.
Rapper huyo ameonekana kuwa karibu na si Babutale tu, bali WCB kwa ujumla kiasi cha kuwepo na dalili kuwa huenda akaungana na akina Rich Mavoko, Raymond na Harmonize. Si jambo gumu kwakuwa kwa muda mrefu Diamond amekuwa akionesha nia ya kumsaidia rapper huyo.
Wakati tukiendelea kumweka Chidi kwenye maombi yetu kama anavyotuomba, tumkumbuke pia dada yetu Ray C ambaye kwa hakika anahitaji maombi zaidi na matumaini mapya.
No comments:
Post a Comment