Monday, 10 October 2016
NECTA yatoa ratiba ya ukaguzi wa vyeti mkoa kwa mkoa
Hatua ya Baraza la Mitihani nchini (Necta) kutoa ratiba ya kufanya uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na ualimu kwa watumishi wote wa umma sasa ni wazi imezidi kupandisha joto kwa vigogo na watumishi mbalimbali ambao hawana sifa za kielimu kushika nafasi walizo nazo.
Katika taarifa yake ya sasa Baraza la Mitihani nchini, limetangaza kuwafuata katika maeneo yao ya kazi watumishi wote walioko katika mamlaka za mikoa, halmashauri na manispaa kwa ajili ya kufanya uhakiki wa vyeti vyao hivyo vya kitaaluma.
Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na Edga Kasuga kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo kwenda kwa Makatibu tawala wa Mikoa, uhakiki utafanyika katika ofisi za Makatibu Tawala wa mikoa kuanzia Oktoba 10 hadi 14 mwaka huu, ingawa ratiba nyingine ya uhakiki imeonyesha zoezi hilo litafikia tamati Novemba 7 mwaka huu.
“Ili kufanikisha zoezi hilo Baraza limetaka kupata orodha (nakala- laini ya soft copy) ya watumishi wote wa umma waliopo katika mkoa, halmashauri na manispaa.
“Nakala za vyeti vya kidato cha nne, cha sita na ualimu vya watumishi wote walioandikishwa na chumba cha kufanyia uhakiki,” inaeleza taarifa hiyo ya Baraza la Mitihani.
RATIBA YA UHAKIKI
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani, uhakiki huo utafanywa katika makundi matano katika mikoa tofauti tofauti.
Oktoba 10, mwaka huu kundi la kwanza litafanya uhakiki katika Mkoa wa Mtwara, kundi la pili Singida, kundi la tatu Rukwa, kundi la nne Katavi na kundi la tano litakuwa Geita.
Oktoba 17 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Lindi, la pili Manyara la tatu Songwe, la nne Kigoma na la tano litakuwa Mwanza.
Oktoba 24 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Morogoro, la pili Arusha, la tatu Mbeya, la nne Tabora na la tano Mara.
Oktoba 31 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Pwani, la pili Kilimanjaro, tatu Ruvuma, la nne Shinyanga na la tano Simiyu.
Novemba 7 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Dar es Salaam, la pili Tanga, la tatu Njombe, la nne Dodoma na la tano Iringa.
JOTO LA UHAKIKI
Kabla Baraza la Mitihani halijatangaza ratiba hiyo, tayari watumishi wa umma ambao wanatumia majina matatu lakini vyeti vyao vya elimu vinasomeka majina mawili walikuwa wamepewa maelekezo ya kwenda kutafuta hati ya kiapo kwa ajili ya kuapa mahakamani ili kuthibitisha majina yao.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili mmoja wa watumishi hao alisema: “Wakati tunaanza kazi sisi ambao vyeti vyetu tulikuwa tunatumia majina mawili shuleni, tuliambiwa tutumie matatu ambayo pia yanatumika hata kwenye ‘salary slip’, sasa tumeambiwa tunatakiwa kwenda mahakamani kuthibitisha.”
Alisema zoezi hilo tayari limeleta changamoto kubwa mbali na kuzua hofu kwa baadhi ya watu ambao taarifa zao za kitaaluma hazipo sawa sawa.
“Mimi binafsi sina hofu zoezi linakwisha kesho lakini kinachoniuma ni kwamba hiyo hati ya kiapo (affidavit) tukienda Mahakama ya Mwanzo tunaambiwa ni lazima tulipie shilingi 10,000 na kibaya zaidi hatupewi risiti lakini kwa watumishi wengine ambao wanafahamiana wanapata huduma bure,” alisema mtumishi huyo.
Tangu Serikali itangaze kuwafuatilia watumishi wake wote wenye vyeti feki hali ya wasiwasi na sintofahamu imetawala miongoni mwa vigogo, maofisa na watumishi wengine ambao vyeti vyao vya kitaaluma haviko sawa sawa au haviendani na kazi au nyadhifa wanazoshikilia.
Source: Mtanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment