Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, amezungumzia sakata la mke wake kudaiwa
kumtukana askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Dk. Mahiga alisema kwamba mke wake alipishana kauli na askari huyo
aliyefahamika kwa jina la Deogratius Mbango, na hakutoa lugha ya matusi
kama inavyodaiwa.
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo, alifuatilia ili kujua ukweli,
ikiwamo kusikiliza sauti ya majibizano baina ya askari huyo na mkewe,
ambapo alibaini kuwa walipishana kauli.
Hata hivyo Balozi Mahiga alisema suala hilo kwa sasa limemalizika na
asingependa kuingia kwenye malumbano zaidi kwa jambo lililopita.
“Ni kweli mama (mke wake) alikuwa katika barabara ya Namanga, ambako
alipishana kauli na askari wa usalama, nami nilifuatilia suala hili kwa
undani sana. Ninachoweza kusema sitaki kuingia kwenye malumbano juu ya
suala hili kwa kuwa limemalizika.
“Wewe umesikiliza hiyo ‘clip’ (sauti ya mazungumzo) je, umesikia neno
tusi? Hilo ndilo ninalojua kwa sasa, mengine sijui yanayoendelea,”
alijibu kwa kifupi Balozi Mahiga.
Alipoulizwa kuhusu kusambaa kwa picha inayomdhalilisha, Dk. Mahiga
alisema kwamba alishangazwa na picha hiyo huku akishindwa kuelewa lengo
la watu walioitengeneza na kuisambaza.
“Hata mimi sijui lengo lao nini kuisambaza ile picha, maana mimi niliiona kama ulivyoiona wewe,” alisema.
Picha ya Balozi Mahiga inayoonyesha suruali yake imelowa sehemu ya
mbele, imekuwa ikizunguka katika mitandao ya kijamii kwa takriban wiki
moja sasa.
No comments:
Post a Comment